Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Machi 19, 2024 Local time: 07:58

Comoros yampoteza msomi, mwanamapinduzi na mwanasiasa Salim Himidi


Salim Himidi akishiriki kwenye maandamano ya wa Komoro mjini Paris
Salim Himidi akishiriki kwenye maandamano ya wa Komoro mjini Paris

Salim Hadji Himidi aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa visiwa vya Comoros, na mwana siasa aliyepigania uhuru wa Comoros amefariki mjini Paris, Ufaransa Jumamosi asubuhi akiwa na umri wa miaka 74.

Himidi alizaliwa Mbeni, visiwani Comoros tarehe 19, April 1945 wakati wazee wake waliporudi nyumbani baada ya vita vya pili vya dunia na kuhitimu masomo ya sekondari katika shule ya King George VI, Zanzibar.

Alisafiri hadi Ufaransa akiwa kijana ambako alisomea historia katika chuo kikuu cha Aix en Provence.

Alirudi Comoros mwaka 1968 na kujiunga mara moja na vita vya uhuru na kuchaguliwa katibu mkuu wa chama cha kisoshalist cha Comoros PASOCO. Alishirikiana na vyama mbali mbali vya kisiasa na vijana katika vita vya kupambana na ukoloni, akijitokeza kuwa moja wapo ya wanasiasa waliopinga vikali sera za Ufaransa kuingilia kati masuala ya Afrika.

Salim Himidi akihojiwa na kituo cha televisheni cha RTMC cha Komoro
Salim Himidi akihojiwa na kituo cha televisheni cha RTMC cha Komoro

Mwanzoni huyu alikataa kushirikiana na Rais Ali Soilihi kabla ya uhuru na hata kupinga mpango wake wa kumpindua Rais wa kwanza wa Comoros, Ahmed Abdallah baada ya kutangaza uhuru wa visiwa hivyo mwaka 1975.

Lakini baada ya mapinduzi ya 1975, alikubali kujiunga na serikali ya mapinduzi ya Ali Soilihi na kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani.

Himidi atakumbukwa kwa kutoa hotuba ya kihistoria, kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wakati Comoros ikijiunga na umoja huo na kutambuliwa kama taifa la visiwa vinne, baada ya Ufaransa kukikalia kisiwa cha Maore kwa nguvu.

Alimwakilishi Ali Soilihi katika mikutano mbali mbali ya kimataifa na kutetea umoja wa visiwa vya Comoros kama visiwa vinne wakati wote. Alifungwa kwa miaka mitatu chini ya utawala wa pili wa Ahmed Abdallah 1978, na kuteuliwa balozi wa nchi za Ulaya chini ya Rais Said Mohamed Djohar. Na mwaka 1997 aliteuliwa tena waziri wa mambo ya nchi za nje na rais Mohamed Taki Abdulkarim.

Salim Himidi (kati kati) kwenye mkutano wa Umoja wa chi za Afrika OAU.
Salim Himidi (kati kati) kwenye mkutano wa Umoja wa chi za Afrika OAU.

Salim Himidi, alihamia Ufaransa mwishoni mwa miaka ya 1990 na kuwa mchambuzi wa vyombo vya habari vya kimataifa ikiwa ni pamoja na Sauti ya Amerika (VOA).

Alikuwa akifanya utafiti juu ya kiunganishi cha chimbuko la lugha ya Kiswahili kutoka pawni ya Afrika ya Mashariki hadi Comoro na Madagascar. Alikuwa pia na kipaji cha kuandika mashairi kilichoonekana katika mawasiliano ya awali ya ukumbi wa ZANZINET mwanzoni mwa enzi ya mtandao.

Alichangia sana kuimarisha uhusiano kati ya Comoros na Tanzania na kutetea uhuru na uzalendo wa mwafrika.

Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika inatoa rambi rambi zake kwa familia, jamaa na marafiki zake wa Comoros na Afrika Mashariki.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Abdushakur Aboud, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG