Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 26, 2022 Local time: 12:05

Uganda na Kenya kushirikiana bila kuzingatia mpaka


Rais Uhuru Kenyatta na Yoweri Museveni wakati wa utiaji saini wa makubaliano yenye lengo la kukuza amani endelevu na maendeleo kati ya jamii za Turkana, Pokot na Karamojong.

Uganda na Kenya zimesaini makubaliano ya ushirikiano ya kuimarisha usalama na amani kwenye mpaka wa nchi hizo mbili katika wilaya za Moroto na Pokot.

Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha ujirani mwema kati ya jamii za wafugaji kutoka nchi hizo mbili, wakiwa na matumaini kwamba hatua hiyo vile vile itaimarisha usalama kwenye mipaka kati ya Uganda, kenya, Ethiopia na Sudan kusini.

Mkataba wa amani ambao kwa kiwango kikubwa unafadhiliwa na umoja wa mataifa, utawanufaisha jumla ya watu milioni nne kutoka jamii za Pokot, Karamoja na Turkana wanaoishi sehemu hiyo ya mpaka wa Kenya na Uganda.

Yaliyomo kwenye mkataba

Kulingana na mkataba huo, Maafisa wa usalama wa Kenya wanalazimika kuwapokonya bunduki wafugaji kutoka jamii ya Pokot, baada ya kuripotiwa kuongeza visa vya wizi wa mifugo na mauaji, hali ambayo imepelekea kuwepo uhasama na migogoro kuongezeka mpakani katika siku za hivi karibuni.

“wakati mlikubali kurudisha bunduki, mauaji hayatokei tena na watoto wenu wanaishi maisha salama bila kuuawa. Zamani watoto walikuwa chakula ya risasi. Walikuwa wanauawa kila siku. Sasa wanakua watu wazima n ahata kuanzisha familia zao. Idadi ya watu hapa sasa imeongezeka” amesema rais wa Uganda Yoweri Museveni.

Serikali ya Uganda, ilifanikiwa kuwapokonya bunduki wafugaji wa Karamojong, na sasa inashutumu wafugaji wa Pokot kutoka Kenya, kuwauzia tena wakaramoja bunduki.

Kuwapokonya wafugaji bunduki

Kati ya bunduki 40,000 zilipatikana kutoka kwa mikono ya wafugaji kati ya nchi hizo mbili, kati ya mwaka 2007 na 2010, idai kubwa ikiwa kutoka kwa wafugaji nchini Uganda.

“huu ni mpango utakaotusaidia sote kuhakikisha ya kwamba tuko na amani, wananchi wetu wanaishi pamoja, na pia kutusaidia kufanya maendeleo ambayo itajumulisha watu wetu pamoja na kuhakikisha ya kwamba hii mipaka haitakuwa tena mipaka ya vita bali itakuwa mipaka ya amani, maendeleo na utajiri” amesema rais wa Kenya Uhuru Kenyatta.

Kenyatta asisitiza umoja bila kuangazia mipaka

Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Uhuru Kenyatta wa Kenya, vile vile wamekubaliana kushirikiana katika kuimarisha huduma za afya, upatikanaji wa maji safi, elimu, biashara na mawasiliano, katika mpangilio ambao raia kutoka sehemu moja ya nchi anaweza kuvuka mpaka na kuhudumiwa katika nchi ya pili bila kuzuiliwa.

“Hii mipaka ambayo tuliletewa na wakoloni, ilikuwa mipaka ya kugawanya watu wetu. Tunataka tuhakikishe ya kwamba tumeondoa hii mipaka ambayo sio yetu ndio wananchi wetu waweze kutembea na mifugo yao kutoka kona moja, kutoka west Pokot hadi hapa Moroto, watu wa Karamoja watoke hapa, wateremke waende hadi Kitale. Hivyo ndivyo tulikuwa tunatembea kabla ya mzungu kufika hapa. Umaskini wetu umeletwa na ujinga wetu wa kusema wewe rudi kwenu, wewe rudi kwako. Hakuna kwa mtu, Afrika ni yetu sisi sote” ameongeza kusema Kenyatta.

Karamoja, Pokot na Moroto ni sehemu zenye hali ngumu ya maisha, wakaazi wakikabiliana na hali ya kiangazi, magonjwa na ukosefu wa chakula kila mwaka.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.

Facebook Forum

XS
SM
MD
LG