Rais Donald Trump akimwita kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un, "Rocket Man" amesema, kiongozi huyo yuko katika safari ya kujitoa muhanga na kusema, dhamira yake ya kuendelea kutengeneza silaha za nuklia na makombora ya masafa marefu kunatishia dunia nzima na kunaweza kusababisha maafa makubwa ya binadamu.
Balozi wa Korea ya Kaskazini alitoka nje ya ukumbi wa mkutano wa UN kabla ya Trump kuwasili na hakuna aliyekuwa kwenye kiti chake hadi hotuba ya dakika 42 ya Rais wa Marekani kumalizika.
Trump alikuwa pia amegadhibika alipoizungumzia Iran akieleza kuwa serikali ya nchi hiyo ni ya kimabavu na inajificha nyuma ya pazia kwa kutumia kisingizio cha demokrasia.
Aliwambia viongozi wenzake waliohudhuria kikao cha ufunguzi cha 72 siku ya Jumannne kwamba, serikali ya Tehran imetumia rasilmali zake muhimu kugharimia makundi ya kigaidi "yanayowauwa Waislamu na kushambulia majirani zake; mataifa yenye amani ya nchi za Kiarabu na Israeli."
Kiongozi wa Marekani alizungumzia pia maswala mengine ya dunia kuanzia vimbunga vya hivi karibuni hadi nadharia yake ya "Amerika Kwanza"