Wakiongozwa na Irene Chepet Cheptai, wanariadha wanawake wa Kenya walionyesha uhodari wa kipekee wa jinsi ya kushindana katika masafa marefu, na kuweka historia, walipochukua nafasi zote sita za juu katika mashindano ya ubingwa wa dunia wa mbio za nyika.
Cheptai aliyewasili Uganda mwishoni mwa wiki akiwa hajashindwa katika mbio za nyika mnamo msimu huu wote, aliwapita wenzake Alice Aprot na Lilian Kassait Rengeruk katika kilomita ya mwisho na kunyakua ushindi kwa kutumia dakika 31 sekunde 57 katika mbiyo hizo za kilomita 10.
Cheptai alisema baadae kwamba mashindano yalikua makali lakini ushindi wao unatokana na kushirikiana pamoja na kusaidiana.
Kwa upande wa wanaume, mkenya mwenzao Goffrey Kamworor alitetea ubingwa wake katika mbiyo za kilomita 12 alipomshinda mwenzake Leonard Barsoton aliyenyakua fedha na methopia Abadi Hadis kuchukua shaba.
Jacob Kiplimo ameipatia Uganda dhahabu yake pekee na ya kwanza aliposhinda za vijana chini ya miaka 20.
Wakikimbia kukiwa na joto kali huko Kampala, Gidey Letesenbet aliokowa Ethopia kwa kiunyakua dhahabu katika mbiyo za vijana chini ya miaka 20, akiwa mwanamke wa kwanza kushinda mara mbili mfululizo katika daraja yake.