Mshukiwa wa shambulizi la bomu lililotokea Jumamosi katika mji wa New York City ambalo liliwajeruhi watu 29 yupo hospitalini akitibiwa majeraha ya risasi baada ya kufyatuliana risasi na polisi.
Waendesha mashtaka wamemfungulia mshukiwa Ahmad Khan Rahami, mwenye miaka 28, mashtaka matano ya jaribio la mauaji kutokana na majibizano ya risasi ambayo yaliwajeruhi maafisa polisi wawili.
Rahami alikamatwa Linden huko New Jersey nje ya Manhattan, saa kadhaa baada ya polisi wa New York kusambaza picha ya Rahami kila mahali wakisema anatafutwa kwa ajili ya kuhojiwa.
Mmiliki mmoja wa mgahawa unaouza pombe huko Linden, alipiga simu polisi jana asubuhi akilalamika kwamba kuna mtu amelala kwenye mlango wake wa biashara.
Maafisa walimtambua mtu huyo ni Rahami, ambaye alifyatua risasi na kuwajeruhi maafisa polisi wawili kabla ya yeye kujeruhiwa.