Wagombea wawili wa kiti cha rais katika visiwa vya Komoro wamekubaliana na uwamuzi wa mahakama ya katiba kwamba matokeo hayawezi kuthibitishwa, jinsi tume ya uchaguzi CENI ilivyotangazwa kutokana na kasoro zilziotokea katika wilaya 13 za upigaji kura.
Akizungumza na Sauti ya Amerika mchambuzi wa masuala ya kisasa mjini Moroni, Mohamed Mchangama anasema ni matokeo ya kipekee lakini jambo zuri ni kwamba wagombea wote wamekubali kuheshimu uwamuzi wa mahakama.
Katika taarifa yake siku ya Jumamosi Mahakama ya Katiba ilieleza kwamba matokeo ya uchaguzi wa duru ya pili yalikua karibu sana kati ya mshindi aliyetangazwa na CENI, Kanali Azali Asoumani na mgombea wa serikali Mohamed Ali Soilihi.
Mahakama inadhani ni muhimu kwa wapiga kura walonyimwa haki zao katika kisiwa cha pili kwa ukubwa cha Nzwani kupiga kura kabla ya mshindi kutangazwa.
Kulikuwepo na wasi wasi katika visiwa hivyo kwamba pindi mahakama itakapobadili matokeo yaliyotangazwa na CENI kutaweza kuzuka ghasia, lakini hali imekua shuari na mgombwa wa upinzani Kanali Azali amesema Jumapili kwamba atakubaliana na uwamuzi wa mahakama kwa ajili ya maslahi ya kitaifa na kushiriki katika marudio ya uchaguzi huo.