Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Pombe Magufuli amefanya mazungumzo na rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta, kando ya mkutano mkuu wa 17 wa kawaida wa wakuu wa nchi wa jumuiya ya Afrika Mashariki na wawili hao kukubaliana kuboresha mahusiano hasa katika nyanja ya kiuchumi.
Miongoni mwa masuala wanayotarajia kutiliwa mkazo ni pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo inayohusisha nchi hizo mbili hasa katika ujenzi wa miundo mbinu, kukuza biashara na kuzalisha ajira kupitia viwanda.
Kwa upande wake rais Kenyatta wa Kenya amesema amefurahi kwa kuona rais wa Tanzania yuko tayari kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili ambao utasaidia katika kumaliza umaskini na kukuza uchumi.
Marais wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Paul Kagame wa Rwanda, Yoweri Museveni wa Uganda na makamu wa rais wa Burundi anayemuakilisha rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunzinza.
Waliokuwa wamealikwa katika mkutano huo ni pamoja na viongozi mbalimbali, akiwemo rais wa Sudan kusini, Salva Kiir, aliyewakilishwa na Makamu wake wa rais.