Wapigaji kura katika kisiwa cha Ngazija huko visiwani Komoro, wamejitokeza kwa wingi kupiga kura Jumapili katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais na gavana, huku wapiga kura wa visiwa vingine viwili, Mwali na Nzuwani walipiga kura kuwachagua magavana wao.
Wafuatiliaji na wachambuzi wanasema uchaguzi unafanyika kwa utulivu na amani, watu wakisubiri kwa mistari mirefu kwenye vituo vya kupiga kura.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon alitoa taarifa Jumamosi jioni akipongeza matayarisho yaliyofanywa na tume ya uchaguzi na kueleza matumaini yake kwamba utafanyika kwa njia ya kuaminika, wazi na huru.
Bw Ban amesema Umoja wa mataifa wa washirika wa Jumuia ya Kimataifa wataendelea kuwasaidia wakomoro katika juhudi zao za kuimarisha demokrasia na kuendeleza maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Kuna wagombea 25 wanaogombania kiti cha rais ambapo watatu watachaguliwa hii leo na wakazi wa kisiwa cha Ngazija. washindi watatu ndio watakaoshiriki katika duru ya pili hapo April 10, pale wakomoro watakapo amua nani atakua rais mpya wa visiwa hivyo vya Bahari ya Hindi.