Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Jumatatu alizindua mikakati mipya ya kukabiliana na rushwa, wizi na matumizi mabaya ya fedha za umma nchini Kenya.
Hatua hiyo inafuatia kujiuzulu kwenye serikali kwa Waziri wake Ugatuzi na Miradi ya Maendeleo Bi. Anne Waiguru baada ya kutuhumiwa kuhusika na wizi wa fedha za umma.
Ripoti maalum kuhusu mbinu mbalimbali za kupambana na tatizo hilo, iliwasilishwa kwa Rais Kenyatta na kamati maalum aliyoiteua majuma kadhaa yaliyopita ili kumshauri jinsi ya kupambana na janga hilo.
Waziri huyo alituhumiwa kwa kupotea kwa zaidi ya shillingi millioni 700 pesa za serikali kwa njia isiyo eleweka .
Akihutubia taifa kwa njia ya televisheni Rais Uhuru Kenyatta amesema maafisa wa serikali wanaohusika na fedha za umma na wale wanaohusika na ununuzi wa bidhaa na matumizi ya serikali watabeba mzigo wa matumizi mabaya ya fedha za umma na ikiwa wanashirikiana na makampuni binafsi yaliyopigwa marufuku na serikali.
“Makampuni binafsi yataanzisha kampeni ya kuhamasisha raia kuhusu maovu ya rushwa na jinsi ni kitendo hiki kilivyo cha aibu na kisichokuwa cha heshima na hasa kwa wale wanaotoa na kupokea rushwa” alisema rais Kenyatta.
Katika siku za hivi karibuni maafisa wakuu wa serikali wamelazimika kujiondoa kwenye nyadhifa zao na wengine wamefikisha mahakamani kwa madai ya kuhusika na rushwa. Baadhi yao ni mawaziri na makatibu wakuu.