Familia za warussia zimeanza utaratibu wa maombolezo na kutambua miili ya waathirika wa ajali iliyotokea jumamosi ya ndage ya Russia nchini Misri. Shirika la habari la Associated Press-AP linaripoti miili 10 ya kwanza kutoka ndege hiyo imetambuliwa.
Msemaji wa wizara ya hali ya dharura nchini Russia, ameiambia AP kwamba jumla ya miili 140 na zaidi ya vipande vya miili 100 vilisafirishwa kwenda St.Petersburg kwa kutumia ndege mbili za serikali hapo Jumatatu na Jumanne.
Abiria wote 224 na wafanyakazi waliokuwemo ndani ya ndege Metrojet Airbus A-321 walifariki wakati ndege hiyo ilipoanguka kwenye peninsula ya Sinai kiasi cha dakika 20 baada ya kuondoka kutoka uwanja wa ndege kwenye eneo la mapumziko la Sharm el-Sheikh nchini Misri kuelekea St.Petersburg. Raia watatu wa Ukrain walikuwa miongoni mwa watu waliokufa.