Mkuu wa majeshi ya Burundi Jenerali Prime Nyongabo, amenusurika kutokana na jaribio la mauwaji alipokua anaelekea kazini katika mji mkuu wa Bujumbura siku ya Ijuma.
Msemaji wa jeshi Kanali Gaspard Baratuza, amesema msafara wa jenerali ulishambuliwa na watu walokuwa na mavazi ya kijeshi watu sita wameuliwa katika shambulizi hilo wakiwemu walinzi watatu washambulizi wawili na raia moja.
Msemaji huyo amesema watu walopanga njama hiyo wanataka kusababisha mgawanyiko katika jeshi la mungano la taifa na kutoa wito kwa utulivu kote nchini.
Burundi imeshuhudia ghasia na mauwaji ya watu mbali mbali tangu mwezi April, pale Rais Pierre Nkurunziza kusema atagombania mhula wa tatu katika uchaguzi ambao hatimae alipata ushindi.
Mkuu mwengine wa jeshi, mshirika wa karibu wa rais wa Burundi, Jenerali Adolphe Nshimirimana aliuliwa mwezi uliyopita katika shambulizi kama hilo la Ijuma.