Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetangaza kusitisha maandamano ya aina yoyote wakati wote wa zoezi la kuchukua fomu za kuwania urais, kutafuta wadhamini mikoani na hata wakati wa kurejesha fomu kwenye tume ya taifa ya uchaguzi.
Uamuzi huo umetokana na kile polisi ilichosema ni sababu za kiusalama, hasa baada ya kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria za usalama barabarani kutokana na misafara mirefu iliyohusisha watu waliokuwa wakitembea kwa miguu, magari, pikipiki na baiskeli wakati wakiwasindikiza wagombea wa vyama vya CHADEMA na CCM.
Naibu mkuu wa jeshi la polisi Tanznaia, Abdulrahaman Kaniki, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam amesema manung'uniko na usumbufu uliojitokeza wakati za zoezi la wagombea urais wa CCM na CHADEMA kuchukua fomu tume ya taifa ya uchaguzi ni miongoni mwa sababu zilizofanya kusitishwa maandamano hayo.
Akizungumzia kuhusiana na uamuzi huo kwamba huenda ukatafsiriwa kuwanyima haki wananchi ya kuamua kushiriki kwenye shughuli za kisiasa, naibu mkuu wa jeshi la Polisi anafafanua zaidi kwamba hizo ni juhudi za kuimarisha usalama.