Rais wa Cuba Raul Catro alifanya ziara fupi huko Vatikan Jumapili ili kumshukuru Papa Francis kwa juhudi zake za kumaliza miongo mitano ya mvutano kati ya Marekani na Cuba wakati nchi hizo mbili zikirudisha uhusiano wa kidiplomasia.
Kiongozi huyo wa Cuba alikutana na Papa mzaliwa wa Argentina kwa karibu saa nzima wakati watu hao wawili wakizungumza katika lugha yao ya asili ya Kihispania.
Papa Francis kiongozi wa kanisa Katoliki duniani alikuwa nguzo muhimu katika mazungumzo ya faragha kati ya Havana na Washington yaliopelekea tangazo la Desemba kwamba nchi hizo mbili zinachukua hatua ya kufungua tena ofisi zao za ubalozi katika miji yao mikuu na kupanua ushirikiano wao wa kiuchumi. Vatikan imesema Papa Francis ambaye ni wa kwanza kutoka Amerika Kusini , binafsi alikua mpatanishi kati ya pande mbili hizo na kuwa mwenyeji kwa wajumbe wa nchi hizo mbili.