Bomu lililipuka Jumatatu kwenye uwanja wa mpira huko Kaskazini mwa Nigeria, dakika chache baada ya rais Goodluck Jonathan kuondoka kwenye mkutano wa kampeni.
Polisi wanasema mlipua mabomu mmoja wa kike alihusika kwenye shambulio la mji wa Gombe. Wafanyakazi wa uokozi wanasema huenda mlipua mabomu wa pili alifariki katika mlipuko huo. Watu 18 walitibiwa kwa majeraha katika hospitali moja mjini humo.
Hakuna aliyedai kuhusika na mlipuko huo, lakini wanamgambo wa Boko Haram wanashukiwa kuhusika kwa sababu wameshambulia eneo hilo mara kadhaa. Jumapili shambulizi la mtu aliyejitoa mhanga katika mji huo liliuwa watu watano.
Wakati huo huo ghasia zimeongezeka Nigeria , huku uchaguzi wa rais wa Februari 14 ukijongea karibu. Wakazi wa mji wa Konduga ulioko jimbo la Borno wameiambia Sauti ya Amerika kwamba wanamgambo wa Boko Haram walishambulia mji huo Jumapili alasiri baada ya kutimuliwa na majeshi ya Nigeria.