Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Mei 28, 2023 Local time: 21:58

Congo yaomboleza kifo cha mjane wa Lumumba.


Patrice Lumumba, waziri mkuu wa Congo akitia saini tangazo la uhuru mjini Leopodville, Congo. Kulia kwake ni waziri mkuu wa zamani wa Ubelgiji Gaston Eyskens, aliyretia saini kwa niaba ya Ubelgiji. Ubelgiji iliitawala Congo kwa miaka 70.

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC – wanaomboleza kifo cha bibi Pauline Lumumba, mjane wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Emery Patrice Lumumba. Bibi Lumumba alifariki usingizini nyumbani kwake Jumanne.

Serikali ambayo imetuma rambirambi za pole kwa watoto pamoja na familia ya bi Lumumba imesema kifo chake ni msiba wa pili kwa taifa baada ya mumewe Patrice Lumumba miaka 53 iliyopita.Hadi kifo chake Pauline Lumumba alikuwa akiishi ndani ya iliyokuwa nyumba na ofisi ya mumewe wakati akiwa waziri mkuu wa Congo.

Pauline Lumumba alishuhudia kukamatwa kwa mumewe mjini Ilebo jimboni Kassai-Occidental kabla ya kuuliwa kwake jimboni Katanga Januari 17, 1961. Barua ya Lumumba kwa Bi-Pauline Aliyoita “risala yangu ya mwisho kwa Pauline” inaaminika na wanahistoria kuwa ni agano kubwa la kisiasa kwa ajili ya vizazi vipya nchini DRC. Kwenye risala hiyo, Emery Patrice Lumumba alisema hahofii maisha yake mwenyewe, ikiwa itahitajika kumwaga damu yake ili wakongo wapate uhuru wa kweli, kamwe hawezi kusita.

Emery Patrice Lumumba alichaguliwa kuwa waziri mkuu wa DRC siku kadhaa kabla ya uhuru wa Kongo Juni 30,1960 kutoka kwa mkoloni wake Ubelgiji. Hadi sasa mazingira aliyouliwa Patrice Lumumba bado hayajafahamika, lakini utafiti unaelezea kwamba kulikuweko na njama ya nchi za magharibi dhidi ya kiongozi huyo.

Miaka miwili iliyopita bunge la Ubelgiji liliomba serikali yao kukubali kuwa ilihusika kwa fikara na mauwaji ya Lumumba.Vilevile inaelezewa kwamba njama hiyo ilipangwa pia na idara za upelelezi za Marekani na Uingereza, lakini hakuna ushahidi wowote wa madai hayo. Kwa kumbukumbu ya Lumumba, serikali ya Congo ilitangaza mwaka uliopita kuwa imeunda mji utakaoitwa Lumumbaville. Mji huo unatarajiwa kuweko huko huko Kassai Mashariki ambako alizaliwa Emery Patrice Lumumba.

XS
SM
MD
LG