Shirika la afya duniani WHO linasema idadi ya waliofariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola imeongezeka kupita watu 7,500 na idadi ya kesi zinafikia 20,000.
Takwimu mpya zilizotolewa Jumatatu zinaonyesha mwelekeo huko Liberia na Guinea ukionyesha kupungua katika maambukizo ya Ebola , wakati kesi za Sierra Leone zikiendelea kuongezeka. Hizo nchi tatu za Afrika magharibi zina karibu idadi ya vifo vyote vya Ebola barani Afrika.
Idadi ya waliofariki katika nchi nyingine iko pale pale huku kukiwa na vifo sita Mali, nane Nigeria na kimoja Marekani. Spain na Senegal kila moja walikuwa na kesi moja ya ugonjwa huo lakini hakuna vifo.
Pia Jumatatu katibu mkuu wa Umoja wa mataifa amesema jumuiya ya kimataifa inahitaji kujiandaa vizuri zaidi kwa mlipuko ujao duniani ambao amesema ndio mtihani ambao kwa hakika utakuja.