Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Aprili 16, 2024 Local time: 11:00

Mashambulizi yazusha wasiwasi Kenya


Afisa wa polisi akilinda maiti za watu sita walouliwa waliposhambulia kambi ya jeshi Mombasa, Kenya Jumapili Nov 2, 2014
Afisa wa polisi akilinda maiti za watu sita walouliwa waliposhambulia kambi ya jeshi Mombasa, Kenya Jumapili Nov 2, 2014

Viongozi wa Kenya walijitokeza Jumapili kulaani vikali mashambulizi na mauaji ya polisi 21 kaskazini mashariki mwa Kenya na mashambulizi mengine mawili katika kambi ya kijeshi mjini Mombasa na kituo cha polisi mjini Malindi.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alitoa onyo kali kwa wafugaji wa County ya Turkana, alipotembelea mji wa Kapedo Jumapili mchana ambako maafisa hao wa polisi waliuliwa walipokuwa wanakwenda kutafuta gari moja la polisi la kupambana na ghasia lililoteketezwa moto karibu na mji huo.

Rais Kenyatta alisema,“silaha ambazo zilichukuliwa kutoka kwa hawa askari, mimi sitaki kuzingoja wiki mbili, nataka mzirudishe leo, lazima mnajua ziko wapi."

Kiongozi huyo wa Kenya aliwaonya pia wale wanaotaka kuwagawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila.

“Kwa wale wanaofikiria watairudisha nchi hii nyuma kwa kutuletea siasa za karne zilizopita hizo hatuelewi sisi. Tunajuwa ya kwamba taifa hili ni la wananchi milioni 40 wa Kenya.”

Kwa upande wake naibu rais William Ruto, alihudhuria misa maalum katika kanisa la Holy Family Basilica, mjini Nairobi, misa iliyofanyika kwa ajili ya familia na marafiki wa maafisa walouliwa na kutoa onyo kwa wanaotaka kuleta vurugu nchini humo.

“Hakuna kundi, hakuna sehemu au genge, litakalowashikilia mateka wakenya, kwa kuchukua silaha na kujipanga na kupigana kuwauwa watumishi wetu wa usalama wakidhani wataachwa bila ya kufanywa lolote. Ninataka kuwaambia, wale wanaotaka kujaribu kupima aina gani ya chuma Kenya imetengenezwa nayo wenyeji au wageni, basi tunawaambia magaidi, washambuliaji mifugo, na wahalifu wote kwamba tutakusanya rasilmali zetu zote ili kuhakikisha tumewafikisha mbele ya sheria na watajibu kila kitendo walicokifanya.

Na huku rais Kenyatta akitembelea eneo la kaskazini mashariki mwa nchi, maafisa wa usalama wa mji wa Mombasa waliripoti kutokea shambulizi lililofanywa katika kambi ya kijeshi huko Nyali mjini Mombasa na watu walokua na visu, mapanga na vilipuzi..

Kamishna wa polisi wa County ya Mombasa, Nelson Marwa aliwambia waandishi habari kwamba huenda washambuliaji ni wanachama wa kundi lililopigwa marufuku la Mombasa Republican council (MRC) linalodai kujitenga na Kenya.

“Itakuwaje kundi la wahalifu wakiwa na akili zao wangelipanga kushambulia kambi ya jeshi katika nchi huru? Kwa hivyo katika shambulizi hilo watu sita waliuliwa kwa risasi na wengine kadha kukimbia wakiwa na majeraha.”

Hata hivyo gavana wa County ya Mombasa Ali Hassan Joho anachukulia mashambulizi hayo kuwa vitendo vya uhalifu.

“Itakuwaje panakuwa na kundi dogo la watu wenye mapanga na visu wanajaribu kushambulia kambi ya kijeshi. Ndio, ni uhalifu mkubwa unaobidi kushughulikiwa, lakini hili suala la hivi sasa, kusema kambi huko Mombasa inashambuliwa, hilo kwa hakika sicho kinachotokea.

Kwa upande wake, Katibu mkuu wa MRC Randu Nzai Ruwa amekanusha katu kwamba kundi lake limehusika.

Na wakati shambulio la Nyali likitokea kulikuwa na shambulio lingine katika kituo kikuu cha polisi cha mji wa Malindi uliyopo kaskazini mwa Mombasa. Naibu mkuu wa polisi mjini huo, kamanda Fredric Mwangi amesema kundi la watu 20 waliokuwa na silaha walijaribu kushambulia kituo hicho cha polisi.

Maafisa wanawasaka waloihusika na mashambulizi hayo ya Malindi na Mombasa.

XS
SM
MD
LG