Maelfu ya wakazi wa Mombasa wakiongozwa na viongozi wao walihudhuria mazishi ya msomi maarufu wa Kenya Profesa Ali Mazrui aliyezikwa katika makaburi ya familia yake mjini Mombasa karibu na jengo la makumbusho la Fort Jesus, siku ya Jumapili.
Mwili wa Profesa Mazrui uliwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mombasa alfajiri na kupokelewa kwa heshima za kitaifa na wakuu wote wa kisiasa wa County ya Mombasa wakiongozwa na Gavana Ali Hassan Joho akiwemo pia Mwanasheria Mkuu wa Kenya, Willy Mutunga.
Mwili wa Profesa huyo ulisindikizwa kutoka New York nchini Marekani na binamu yake Profesa Al Amin Mazrui, mjane wake Pauline Uti, kijana wake Farid na wenzake wawili wa chuo kikuu cha Binghamton New York.
Profesa Mazrui alifariki Oktoba 12, 2014 nyumbani kwake Vestal, New York baada ya kuugua kwa muda fulani akiwa na umri wa miaka 81.