Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, amesema ukuwaji wa haraka wa uchumi wa nchi za Afrika haujaweza kuwanufaisha wananchi walo wengi kwa sababu ukuwaji wa sekta ya kilimo ambayo wananchi wengi wanategemea haijakua kwa haraka.
Akizungumza katika jopo la wataalamu wa kimataifa lililotayarishwa na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Marekani, USAID, hapa Washington siku ya Ijuma Rais Kikwete anasema, ingawa ripoti mpya ya Benki Kuu ya Dunia juu ya "Kukomesha ufukara ulokithiri na kuhamasisha ukuwaji" inaeleza kwamba ufukara duniani umepunguka kwa kasi mnamo miongo mitatu iliyopita, lakini anasisitiza kwamba wananchi wa Afrika hawajashuhudia mabadiliko hayo ya haraka.
Kiongozi huyo wa Tanzania, aliyewasili Marekani kuhudhuria mkutano wa viongozi wa Umoja wa Mataifa anasema mengi yanahitajika kufanywa ili kuweza kubadili hali hiyo kwa kuwekeza zaidi katika kilimo.
Na katika hafla nyingine iliyoandaliwa na Watanzania wanaoishi Marekani pamoja na wanachama wa chama tawala cha Tanzania cha CCM, Rais Kikwete, alieleza furaha yake kutokana na kwamba pendekezo lake la kuwataka Watanzania, hapa Marekani kuungana na kuunda vikao vya mashauriano na kusaidiana limetekelezwa kupita alivyo tarajia.
"Usiku wa Jakaya" ni hafla iliyoandaliwa hasa na wanachama wa CCM ili kumpongeza kiongozi wao kutokana na mafanikio aliyoyafanya mnamo miaka 10 ya utawala wake wa awamu ya nne Tanzania.
Kaika hotuba yake kwenye ukumbi wa hoteli ya JW Marriot mjini Washington, Rais Kikwete alizungumzia kwa urefu mafanikio katika miundo mbinu, kuimarishwa uchumi, elimu afya na huduma za jamii. Lakini alisisitiza kwamba lengo kuu lililobaki ni kuhakikisha maisha bora kwa wananchi wote wa Tanzania, na kupambana na ufukara.