Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Machi 29, 2024 Local time: 11:28

Maaskofu Congo wamtaka Kabila asibadili katiba.


Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila akizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo Joseph Kabila akizungumza na waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry.

Mjadala mkali umeibuka baada ya maaskofu wa kanisa katoliki nchini Kongo kumuomba rais Joseph Kabila kutobadili katiba ya nchi hiyo ili kumruhusu kuwania muhula wa tatu.Upinzani umelezea kwamba msimamo huo wa maaskofu ni jibu muafaka la njama ya chama tawala kutaka rais Kabila aendelee kubaki madarakani,huku chama tawala kikiwa na tafsiri nyingine ya ujumbe huo.

Bado chama tawala hakijatoa msimamo wake rasmi kuhusu tangazo la maskofu wa kanisa katoliki la kumtaka rais Joseph Kabila kutowania muhula wa tatu ifikapo mwaka wa 2016.Lakini baadhi ya wabunge na vigogo wa chama wamepokea kwa shingo upande pendekezo hilo la maaskofu wa kanisa katoliki.Mbunge Shiko Mwepu amesema kwamba maaskofu hao wameunga mkono jumuiya ya kimataifa katika dhana zisizokuwa na msingi wowote, kwake yeye ni kwamba viongozi hao wa kanisa wamejiingiza katika siasa. "Ikiwa wanataka kufanya siasa basi wavue kanzu ", alisema mbunge huyo kutoka jimbo la Katanga .

Kwa upande wake upinzani umepongeza msimamo huo wa maaskofu,Vital Kamerhe kiongozi wa chama cha UNC ameandika kwenye mtandao wa Twita kwamba maaskofu wametaka kunusuru demokrasia kutokana na njama ya wanasiasa wa chama tawala.Katibu mkuu wa Kongamnao la maaskofu na ambaye ni msemaji wake,padre Leonard Santedi amewambia wandishi habari kwamba ni muhimu katiba itekelezwe.

"Tumeliomba bunge kujizuia na kupitisha miswaada ya sheria ambayo inaweza kuhujumu katiba na taratibu ya kidemokrasia nchini hapa".

Ombi hilo linaelezewa na maaskofu hao kuwa ni juhudi za kuweko na mageuzi ya kidemokrasia nchini Kongo.Katiba ya Kongo inaelezea kwamba rais amechaguliwa na raia kwa muhula wa miaka mitano na anaweza kuwania tena muhula wa pili na wa mwisho.Kipengele hicho kimebanwa na kile cha 220 ambacho kinaelezea kwamba mfumo wa uchaguzi,uwingi na kipindi cha mihula ya rais havipaswi kurekebishwa kwa sababu yeyote ile.Claude Kayembe ni mwandishi habari na ameelezea jinsi ujumbe huo wa maaskofu unapokelewa na raia wa Kongo

Hata hivyo maaskofu hao wameunga mkono tume ya uchaguzi CENI ili kuendelea na shughuli zake za maandalizi ya uchaguzi na vilevile serikali imepongezwa katika kurejesha amani huko Kivu.

Hadi sasa rais Kabila bado kutangaza msimamo wake kuhusu mjadala uliojitokeza kuhusu swala la kubadilishwa kwa katiba na vilevile ikiwa atawania muhula wa tatu au hapana.Msemaji wa serikali ya Kongo Lambert Mende amesema bila shaka rais kabila ataheshimu katiba.Mende aliendelea kusema kwamba bado rais Kabila ana miaka 2 na nusu ya kuongoza nchi hiyo kwa hiyo swala la kujua ikiwa atagombea au hapana haliko kwenye ajenda ya serikali kwa sasa. Mende amelezea misimamo ya hapa na pale kuhusu mageuzi ya katiba ni dhana ya watu binafsi.

Wakati wa ziara yake mjini Kinshasa mwanzoni mwa mwezi Mei,waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry aliwaambia waandishi wa habari kwamba miongoni mwa maswala waliozungumzia na rais kabila ni pamoja kumuomba kutobadili katiba.Haijulikani jibu la rais lilikuwa ni lipi ?

XS
SM
MD
LG