Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Mei 18, 2024 Local time: 04:23

Tanzania yasema italinda mipaka yake,.


Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete akiwa na mkuu wa majeshi Jeneral Davis Mwamunyange. REUTERS/E
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete akiwa na mkuu wa majeshi Jeneral Davis Mwamunyange. REUTERS/E
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete amesema kuwa yeyote ambaye atajaribu kuchezea usalama na mipaka ya Tanzania atakiona cha mtema kuni. Rais Kikwete alitoa matamshi hayo leo wakati akihutubia katika maadhimisho ya siku ya kumbukumbu ya mashujaa katika mkoa wa Kagera unaopakana na Rwanda.

Rais Kikwete alisema Jeshi Tanzania liko imara tayari kulinda mipaka ya Tanzania wakati wowote na saa yoyote. Matamshi hayo yametolewa huku kukiwa na mvutano wa chini chini kwa wiki kadhaa sasa kati ya Rwanda na Tanzania.

Mvutano huo umetokana na kauli ya Rais Kikwete mwezi Juni ya kuitaka Rwanda kufanya mazungumzo na waasi wa FDLR wa Rwanda ambao walikimbilia nchini DRC. Kauli hiyo ilimkasirisha rais Paul Kagame wa Rwanda aliyediriki kusema akikutana na mtu aliyetoa matamshi atampiga.

Tangu hapo nchi hizo zimekuwa na mvutano wa chini kwa chini na hali ya kukwepana katika mikutano ya kimataifa, hata ile inayohusisha maswala ya nchi za afrika mashariki wakati nchi zote mbili ni wanachama wa jumuiya ya afrika mashariki.

Katika hotuba yake iliyotolewa baada ya kutembelea makaburi ya askari wa Tanzania waliopoteza maisha yao wakati wa vita vya Tanzania na Uganda 1978/79 rais kikwete aliwaambia wananchi wa mkoa wa kagera:

“Laleni usingizi salama. Msisikilize maneno ya mitaani kwa sababu Jeshi letu liko imara kabisa kulinda nchi yetu na mipaka yake. Yeyote atakayejaribu kuivamia ama kuichokoza nchi yetu atakiona cha mtema kuni. Nchi iko salama na Jeshi liko imara kulinda nchi yetu,”

Rais Kikwete aliongeza kuwa:
“Ujumbe wetu mkubwa wa leo ni kwamba tuko tayari wakati wote na, saa yeyote kuilinda nchi yetu na mipaka yake. Hatuna nchi nyingine. Hivyo, kamwe hatuwezi kumruhusu yeyote kuicheza nchi yetu, ama kuichezea ama kuimega nchi hii. Kama tulivyoshughulika na Amin naye tutashughulika naye vivyo hivyo.”

Wachumbuzi wa siasa wanasema matamshi ya kikwete leo bila shaka yalilenga kutuma ujumbe kwa Rwanda kufuatia matamshi makali makali ambayo rais wa nchi hiyo amekuwa akiyatoa kupinga ushauri wa rais kikwete.

Katika mkutano wa nchi za maziwa makuu kando ya mkutano mkuu wa umoja wa afrika mwezi juni, rais kikwete alipendekeza nchi za Uganda, Rwanda na DRC zianze mazungumzo na waasi wa nchi hizo kama hatua ya kutafuta suluhisho la kudumu.

Rwanda ilichukizwa sana na kauli hiyo, ikisema kwamba kamwe haiwezi kukaa katika meza ya mazungumzo na waasi wa FDLR ambao walihusika katika mauaji ya jumla nchini Rwanda mwaka 1994.
XS
SM
MD
LG