Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Machi 25, 2023 Local time: 18:00

Bunge la Tanzania lapitisha azimio dhidi ya shambulizi la Arusha.


Bunge la Tanzania mjini Dodoma.
Kufuatia kutokea kwa shambulio la bomu jijini Arusha, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha Azimio la kuitaka serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua mara moja dhidi ya viashiria vya aina zote vya uvunjifu wa amani unaojitokeza nchini humo.

Akitoa azimio la bunge la kulaani tukio la kulipuliwa kwa bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi Parokia ya Olasiti jijini Arusha, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ulinzi na Usalama, Bibi Anna Abdallah, alisema serikali inatakiwa kufanya uchunguzi wa kina dhidi ya tukio la kigaidi la Arusha lililoua watu watatu na wengine zaidi ya 60 kujeruhiwa.

Wabunge mbalimbali walipata nafasi ya kuchangia hoja hiyo kabla ya kuipitisha kwa kauli moja.

Baadhi ya wabunge wa upinzani walikuwa Kabwe Zitto Kigoma Kaskazini CHADEMA na James Mbatia mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa taifa wa NCCR MAGEUZI.

George Simbachawene mbunge wa Kibakwe, CCM pamoja na Dakta Getrude Lwakatare, mbunge wa viti maalum CCM kwa pamoja walisisitiza kwa viongozi na watu wengine wenye nafasi kuacha kutoa matamko yanayowagawa watanzania.

Nao wabunge kupitia Spika Bi. Anne Makinda, wameamua kutoa posho yao ya siku moja kwa ajili ya kuwafariji wahanga wa shambulio hilo, na kutuma ujumbe.

Wakati huo huo mkuu wa mkoa wa Arusha ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wale washukiwa wanne waliokamatwa kuhusiana na mlipuko wa mabomu ya Arusha watatu kati yao ni raia wa Falme za Kiarabu na si Saudia Arabia kama ilivyotangazwa awali.

Wizara ya mambo ya nje ya Falme za Kiarabu imethibitisha kwamba raia wake watatu wamekamatwa nchini Tanzania na kusema wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya kesi hiyo.
XS
SM
MD
LG