Kiongozi wa waasi wa kundi la M23 amesema Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inastahili kulaumiwa kutokana na kuvunjika mazungumzo ya amani yaliyofanyika nchi jirani ya Uganda.
Mazungumzo hayo yalifuatia makubaliano ya viongozi katika mkutano wa kimataifa kwenye nchi za maziwa makuu kusaidia kumaliza ghasia mashariki mwa DRC.
Bertrand Bisimwa alisema Kinshasa haikuwakilishwa Kampala , Lakini ujumbe wao uko Kampala na ukisubiri serikali ya Kinshasa kurejea na pengine kuweza kuendelea na mazungumzo.
Anasema wanachama wa kundi lake wanakerwa na serikali ya DRC kushindwa kutimiza ahadi zake katika mazungumzo.
Bisimwa alisema M23 inataka msamaha kwa wapiganaji wake wote lakini serikali bado haijatekeleza madai yao.
Bisimwa pia alikanusha kwamba kundi lake linapata msaada kutoka Uganda na Rwanda.