Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 03, 2023 Local time: 04:41

Kiwanda cha mbolea chalipuka Texas.


Mabaki ya kiwanda cha mbolea kilicholipuka katika mji wa Waco, Texas.
Mabaki ya kiwanda cha mbolea kilicholipuka katika mji wa Waco, Texas.
Maafisa katika jimbo la kusini magharibi la Texas nchini Marekani wanasema zaidi ya watu 100 wamejeruhiwa baada ya kiwanda cha mbolea kulipuka jana jioni karibu na mji wa Waco. Taarifa za habari zinasema watu kadhaa wamekufa lakini maafisa hawajatoa idadi kamili ya waliofariki.

Mlipuko ulitokea wakati kikosi cha zimamoto kwenye mji mdogo wa west walipokuwa wanajaribu kuzima moto katika kiwanda hicho muda mfupi kabla ya usiku kuingia. Afisa mmoja kutoka idara ya usalama wa umma huko Texas anasema kati ya nyumba 50 hadi 75 karibu na kiwanda hicho zimeharibiwa.

Wakazi wengi katika eneo hilo waliondolewa wakiwemo zaidi ya wazee 100 katika nyumba moja ya kuhifadhi wazee ambayo iliharibiwa vibaya na mlipuko huo. Kundi la uokozi lilianza kufanya msako wa nyumba kwa nyumba katika eneo hilo kutafuta kama kuna mtu aliyekwama ndani.

Afisa mmoja kutoka idara ya polisi mjini Waco anasema baadhi ya wafanyakazi wa zimamoto kutoka mji wa west hawajulikani walipo.

Kundi lingine la uokozi kutoka dazani za miji ya karibu na vitongoji liliitwa kusaidia katika janga hilo. Gavana wa Texas, Rick Perry alisema rasimali za jimbo zimeandaliwa kusaidia maafisa wa ndani.
XS
SM
MD
LG