Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumapili, Desemba 04, 2022 Local time: 15:54

Msanii maarufu Bi.Kidude afariki dunia


Bi Kidude enzi za uhai wake.
Msanii Mkongwe Zanzibar Fatma binti Baraka maarufu ‘Bi Kidude’ amefariki dunia Jumatano saa sita mchana na kuacha pigo kubwa kitaifa na kimataifa katika fani ya unyago na muziki wa Taarab.

Bi Kidude amefariki akiwa na umri upatao 103, na anatarajiwa kuzikwa kesho katika kijiji Kitumba, kilichopo Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja.

Mara baada ya kupatikana kwa taarifa za kifo cha msanii huyo Mkongwe, watu mbalimbali walianza kukusanyika nyumbani kwake Mtaa wa Raha leo, wengine wakishindwa kujizuia kutokwa na machozi.

Akizungumza na idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika msemaji wa familia, Baraka Abdallah Baraka amesema marehemu Bi Kidude alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya sukari, mapafu na figo na hali yake ilizorota ghafla mchana na kufariki dunia akiwa chini ya uangalizi wa wanafamilia huko Bububu.

Baadhi ya wasanii waliokuwa karibu na marehemu Bi Kidude, akiwemo Maryam Hamdan pamoja na Makame Faki Makame, wamesema wamepokea taarifa za kifo hicho kwa mshtuko mkubwa, na kamwe hawatamsahau kutokana na umahiri wake mkubwa uliomjengea heshima kitaifa na kimataifa.

Bi Kidude atakumbukwa kwa mchango mkubwa aliouacha, ambapo ameweza kushiriki katika matamasha mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, na kuzoa tunzo nyingi, ikiwemo kuweza kuimba akiwa na umri mkubwa jambo ambalo limempa umaarufu mkubwa na kuwa kivutio katika maonesho yake.
XS
SM
MD
LG