Watu wanne wamethibitishwa kuwa wamefariki dunia na wengine 18 wamejeruhiwa vibaya baada ya jengo la ghorofa 16 kuporomoka katikati ya jiji la Dar es salaam.
Jengo hilo liliporomoka majira ya saa mbili asubihi ijumaa wakati shughuli za kikazi zikiwa zinaendelea. Mashahidi wanasema inakadiriwa kuwa kulikuwa na watu kati ya 30 hadi 60 ndani ya jengo wakati ajali hiyo inatokea.
Inasadikiwa kuwa kulikuwa na watoto wa shule ya Madrasa katika msikiti wa Shia waliokuwa karibu na jengo hilo linalojengwa na kampuni ya ukandarasi ya Lucky Cnstruction LTD.
Hata hivyo taarifa za awali zinasema kulikuwa na wakati mgumu wa kuokoa watu waliokuwa wamefunikwa katika kifusi cha jengo hilo kwa sababu ya kutokuwepo vitendea kazi sahihi.
Juhudi za uokozi zinaendelea katika eneo hilo lililo maarufu kwa harakati nyingi. Kamanda wa polisi kanda maalumu jijini dar es salaam Suleiman Kova amewataka wananchi kuwa na subira wakati wanajaribu kuchimbua kifusi.
Miongoni mwa viongozi wengine waliofika katika tukio hilo ni pamoja na rais Jakaya Kikwete, mkuu wa mkoa wa dar es salaam Sadid Meck Sadik.
Janga hili limetokea wakati wakazi wakiwa katika harakati za maandalizi ya sikuu ya pasaka ambayo kwa wakristo inaanza rasmi Ijumaa kuu .