Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Machi 28, 2024 Local time: 14:45

Marekani kufanya mageuzi katika sheria za uhamiaji


Mwanamke akiwa na bango la kutetea wahamiaji nje ya ubalozi wa Marekani, Mexico City.
Mwanamke akiwa na bango la kutetea wahamiaji nje ya ubalozi wa Marekani, Mexico City.
Kundi la maseneta wanane kutoka chama cha Democrat na Republican nchini Marekani Jumatatu lilieleza kufikia makubaliano katika pendekezo la mfumo wa kubadili sheria za uhamiaji. Rais Barack Obama anategemewa kufafanua maono yake juu ya pendekezo hilo katika hotuba Jumanne akiwa Nevada.

Wabunge hao walisema makubaliano yao yalijikita katika maswala magumu lakini ya kimsingi ambayo rais Obama ameunga mkono kwa muda mrefu kuelekea kuwapa uraia wahamiaji milioni 11 ambao wanaishi Marekani kinyume cha sheria.

Mpango huo unatoa maelezo mahsusi ambayo sharti yatimizwe na wahamiaji wasio halali kabla ya kupewa uraia wa Marekani. Wahamiaji wanaotafuta ukazi wa kudumu maarufu kama Green Card ili waweze kufanya kazi wanatakiwa kutimiza masharti kadha kama vile kulipa kodi na faini zozote ambazo wametozwa na ni lazima waweze kuzungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha.

Miongoni mwa maswala ambayo rais Obama ametetea ni kuhalalisha watoto wa wahamiaji wasio halali ambao wamesoma Marekani. Wengine wao walizaliwa Marekani au walikuja na wazazi wao wakiwa wadogo na hawatambui nchi za wazazi wao. Watoto kama hao mara nyingi hukabiliwa na adhabu ya kurejeshwa katika nchi walikotoka wazazi wao wasio halali.

Katika hotuba yake alipokula kiapo kuongoza Marekani muhula wa pili, rais Obama alisema; “safari yetu haitakamilika hadi pale tutakapobaini njia nzuri ya kuwakaribisha wahamiaji wanaoiona Marekani kama nchi ya fursa na matumaini.. hadi pale wanafunzi werevu na wahandisi watakapopata nafasi inayostahiki, kuliko kuwafukuza Marekani”.

Lakini kungali na upinzani mkubwa wa pendekezo hili. Rosemary Jenkins wa kundi la Numbers USA anasema kuhalalisha wahamiaji wasio halali kutapeleka ujumbe kwa dunia kwamba “unaweza kuja Marekani kinyume cha sheria,ukavunja sheria kwa muda mrefu na baadaye ukatunukiwa zawadi ya kuishi Marekani kisheria.
XS
SM
MD
LG