Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 02, 2024 Local time: 01:11

Treni ya kisasa Kenya kuboresha uchumi wa Afrika Mashariki


Safari ya kwanza ya majaribio kwa treni mpya Kenya
Safari ya kwanza ya majaribio kwa treni mpya Kenya

Treni ya kisasa imefanya majaribio nchini Kenya Alhamisi ambayo inaunganisha miji ya Mombasa, Nairobi na nchi jirani ya Uganda.

Reli hiyo itafungua milango mipya kwa wananchi wa nchi hizo katika nyanja mbalimbali na hivyo kukuza uchumi wa Kenya na nchi jirani.

Kufikia sasa Kenya imepokea treni 12 zikiwapo sita za kubebea abiria, zilizowasili mwishoni mwa Januari katika bandari ya Mombasa. Treni hizo zimenunuliwa na serikali ya Kenya kutoka China.

Mwandishi wa Idhaa ya Kiswahili VOA ameripoti kuwa mradi huo umeigharimu serikali takriban dola bilioni 4 inatarajiwa utakapomalizika, treni hizo zitakuwa na uwezo wa kubeba takriban abiria elfu tatu kila siku.

Muda wa safari sasa ni saa nne

Amesema kuwa safari za kutoka Mombasa hadi Nairobi zitachukuwa saa nne wakati hivi sasa usafiri wa mabasi unachukuwa takriban saa nane.

Pia ameongeza kuwa maeneo ambayo inapita reli hiyo ni pamoja na Changamwe Small, Voi, Mutito-Andei, Syokimau, hadi Nairobi na kueleza kuwa ni maeneo ambayo yanatoa ajira nyingi hivyo kuwawezesha watu kupata unafuu wa kimaisha.

Wachambuzi wa kibiashara wamesema kuwa kuwepo wa treni hizi za mwendo kasi zitawawezesha wananchi kufanya biashara katika nchi jirani za Uganda na Rwanda siku za usoni.

Katika safari yake ya kwanza ya majaribio treni hiyo ilianza safari yake mapema Alhamisi katika mji wa Mombasa na shughuli ya kukagua reli hii inatarajiwa kuanza wiki ijayo katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi.

Uzinduzi kufanyika mwezi Juni

Kamishna mkuu eneo la Pwani, Nelson Marwa amewaambia waandishi wa habari kuwa uzinduzi rasmi wa treni hizo utafanyika mapema mwezi Juni, ambapo Rais Uhuru Kenyatta atazindua safari za Nairobi kwenda Mombasa.

“Uzinduzi huu ni dalili njema kuwa magari moshi haya yataanza kufanya kazi ifikapo mwezi wa sita,” Marwa alisema.

“Tumehakikisha kuwa magari haya yamefika mapema ile tuwe na muda wa kutosha wakukagua reli hii ya kisasa kabla ya mwezi Juni.” Meneja mkuu wa shirika ya reli nchini Kenya Atanas Maina alisema.

Hadi sasa magari 12 yamefika nchini Kenya huku ikitarajiwa kuwa ifikapo mwaka 2018, mradi huo wa serikali ya Kenya utakuwa na magari moshi 52.

Kwa sasa Reli hiyo imejengwa kutoka Mombasa hadi mji mkuu Nairobi, na awamu ya pili itashuhudia ujenzi ukiendelea hadi Nakuru, katika mkoa wa bonde la ufa.

Hatimaye relihiyo itajengwa ili kuuanganisha Kenya na mataifa jirani ya Uganda, Rwanda na Sudan Kusini.

XS
SM
MD
LG