Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Mei 08, 2024 Local time: 23:17

Serikali ya Tanzania yakiri elimu finyu imechangia mzozo wa gesi Mtwara


Maandamano ya wakazi wa Mtwara katika suala la uchimbaji gesi Mkoani humo
Maandamano ya wakazi wa Mtwara katika suala la uchimbaji gesi Mkoani humo
Mgogoro wa gesi asilia mkoani Mtwara nchini Tanzania bado unagonga vichwa vya wanasiasa wakati Waziri Mkuu nchini humo Mizengo Pinda akizungumzia kusudio la kutoa taarifa bungeni juu ya muafaka uliofikiwa ili kuona kama bado ipo haja kwa bunge kuendelea kuunda tume maalum ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

please wait

No media source currently available

0:00 0:02:35 0:00
Kiungo cha moja kwa moja

Taarifa ya bwana Pinda imekuja siku moja tu baada ya spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda kuliambia bunge azma ya kuunda tume maalum ya kwenda mkoani Mtwara kusikiliza na kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo wa gesi.

Katika mkutano wake na wandishi wa habari mjini Dodoma uliozungumzia jitihada alizofanya kulitafutia ufumbuzi suala la mgogoro wa gesi, Waziri Mkuu amekiri kwamba tatizo kubwa lililozua mgogoro huo ni kwamba wananchi wa mkoa huo hawakupewa elimu ya kutosha juu ya utekelezaji wa mradi wenyewe wa gesi.

Bwana Pinda amewataka viongozi wa ngazi zote katika mkoa wa Mtwara kuwashirikisha wananchi katika kila hatua ya mradi wa uchimbaji wa gesi hiyo asilia ili wananchi hao waweze kunufaika na fursa za mradi huo.

Katika ziara yake mkoani humo Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi hao kuwa kiwanda cha kusafisha gesi ghafi kitajengwa mjini Mtwara, kwa hiyo hawana budi sasa kujipanga vyema kuzitumia fursa zitakazojitokeza kupitia mradi huo mkubwa.

Wakati huo huo Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Bwana Emmanuel Nchimbi amewataka wananchi kuelewa kwamba uharibifu wa mali za serikali wakati wa vurugu ni hasara yao kwavile mali hizo zimewekwa hapo kupitia kodi zao mbalimbali.

Alisema vurugu zilizotokea katika maeneo ya mtwara mjini na wilayani Masasi, tathimini ya awali inaonyesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imepata hasara ya mali zenye thamani ya shilingi bilioni 1.5 na ili halmashauri hiyo iweze kurejea kufanya kazi zake, kiasi cha shilingi milioni 791 zinahitajika.

Katika habari nyingine jijini Dar Es Salaam, Rais Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-DRC aliwasili nchini kwa ziara ya siku moja ambapo atakuwa na mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. Rais Kikwete ni mwenyekiti wa asasi ya ulinzi na usalama ya jumuiya ya maendeleo ya kusini mwa afrika-SADC kitengo kinachoshughulikia pia mgogoro wa kisiasa mashariki mwa Congo.
XS
SM
MD
LG