Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Aprili 27, 2024 Local time: 01:33

Obama kukamilisha ziara Tanzania Jumanne


Rais Obama akagua gwaride la heshima alipowasili Dar- es-Salaam, Tanzania.
Rais Obama akagua gwaride la heshima alipowasili Dar- es-Salaam, Tanzania.
Rais wa Marekani Barack Obama na rais wa zamani wa Marekani George W. Bush ambaye pia yumo Tanzania, leo Jumanne wataweka shada la maua katika eneo lililokuwa zamani ubalozi wa Marekani mjini Dar-es-Salaam na ambao ulishambuliwa na magaidi wa al-Qaida mwaka wa 1998.

Jana rais Obama na mwenyeji wake rais wa Tanzania Jakaya Kikwete walijadilia mipango ya kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi baina ya Marekani na Afrika pamoja na mpango mpya wa Marekani kutoa msaada barani humo.

Familia ya rais Obama ilipata makaribisho ya kipekee ilipowasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jumatatu na kutumbuizwa kwa ngoma za kienyeji na bendi ya kitamaduni pamoja na wanawake waliovalia Khanga zenye picha ya rais Obama.

Katika mazungumzo ya pamoja marais hao wawili walizungumzia ushirikiano wa kibiashara, maendeleo na uwekezaji.Bw.Obama alikariri mpango wake mpya wa mahusiano baina ya Marekani na Afrika

Naye Rais Kikwete alimshukuru rais Obama kwa kuunga mkono juhudi za maendeleo Tanzania ikiwemo elimu, usalama wa chakula na program za kudhibiti viruysi vya HIV na Ukimwi.

Bw.Obama alisema Tanzania ni mshirika wa karibu wa Marekani katika miradi mbalimbali na kuipongeza kwa juhudi ilizofikia za kidemokrasia.

Viongozi hao wawili pia wajadilia mitafaruku barani Afrika, ikiwemo mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Bw. Obama alisema pande zote zinatakiwa kutekeleza makubaliano ya amani yaliyofikiwa majuzi chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Wakati huo, huo, mke wa rais Obama, Michelle Obama na mke wa rais wa zamani Laura Bush, watashiriki katika kongamano kuu la Wake wa marais jijini Dar-es-Salaam unaolenga kujadilia njia za kuwawezesha wanawake wa Afrika.

Rais Obama na ujumbe wake watazamiwa kuondoka Tanzania mwendo wa saa sita adhuhuri kwa saa za Afrika Mashariki leo Jumanne.
XS
SM
MD
LG