Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Mei 02, 2024 Local time: 01:11

Maseneta wa Marekani wapendekeza kupitishwa kwa mswaada.


Wizara ya mambo ya nje ya Marekani inasema inatafakari juu ya kuorodhesha tawi la Taliban nchini Pakistan katika makundi ya kigeni ya kigaidi.

Maafisa hapa wanasema utaratibu wa kuliorodhesha kundi la Taliban huko Pakistan kama kundi la kigaidi tayari umeshaanza, na utamalizika hivi karibuni, na kwamba hakuna haja ya kuwekwa sheria juu ya suala hilo.

Matamshi hayo yalitolewa baada ya maseneta wanne wa Marekani kusema kuwa watawasilisha mswaada utakaohitaji hatua hiyo kuchukuliwa.

Walichukuwa hatua hiyo siku moja baada ya raia wa Marekani mwenye asili ya kipakistan Faisal Shahzad, kusema katika mahakama ya New York, kuwa alipokea fedha na mafunzo ya kutengeneza bomu kutoka kwa kundi la Taliban la Pakistan, katika jaribio lake la kuripua gari mwezi ulopita katika mtaa wa Times Square.

Akijiita askari wa kiislamu, Shahzad alikiri makosa ya mashtaka kumi ya ugaidi na mashtaka mengine ya kuwa na silaha, baada ya kuacha bomu ambalo halikuripuka katika eneo mashuhuri kwa watalii hapo Mei mosi.

Maseneta hao walisema walifikisha ombi kwa waziri wa nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton, kuliweka kundi hilo kwenye orodha ya Marekani ya makundi yakigaidi wiki kadhaa zilopita.

Wanasema kufwatia kukiri makosa kwa Shahzad, huu ni wakati wa kuchukwa hatua nyengine ya kukabiliana na kundi lilomsaidia.

Kuna makundi 45 ya kigaidi katika orodha ya wizara ya nchi za nje ya Marekani.

Kuwepo kwenye orodha hiyo, kunapelekea kuzuiliwa kwa mali yote ya makundi hayo yaliopo Marekani, kuwekewa vikwazo vya usafiri na vya kifedha kwa wanachama wake na kunakufanya kuwa kosa kuwapatia misaada ya vifaa.

Seneta mdemocrat wa New York Charles Schumer, ambaye anaunga mkono pendekezo la sheria hiyo, anasema kundi la Taliban huko Pakistan ni tishio kwa wanajeshi wa Marekani waliopo nje na wananchi hapa nyumbani, na kwamba huu ni wakati wa kutumia mbinu zote dhidi yao.

Maseneta wengine walounga mkono mswaada huo ulopendekezwa ni wademokrat seneta wa New york Kirsten Gillibrand, na maseneta Robert Menendez na Frank Lautenberg wa New Jersey.

XS
SM
MD
LG