William Ruto aapishwa rais wa tano wa Kenya

Kenya Election

William Ruto ameapishwa kama rais wa tano wa Kenya  siku ya Jumanne, wiki moja baada ya Mahakama ya Juu kuidhinisha uchaguzi ambao ulikatiza matumaini ya familia mashuhuri za kisiasa nchini humo  na kumpa mamlaka mtu ambaye alianza kazi yake kama muuza kuku kando ya barabara.

Ruto, ambaye alihudumu kama naibu wa rais wa Kenya kwa miaka 10, anachukua hatamu za uongozi wakati wa bei za vyakula na mafuta ziko juu, ukosefu mkubwa wa ajira na kuongezeka kwa deni la umma.

Kufikia saa kumi na moja alfajiri uwanja wa michezo wa Kasarani jijini Nairobi wenye uwezo wa kuchukua watu 60,000 ulikuwa umejaa wafuasi wa Ruto waliovalia rangi za njano na kijani za chama chake. Walicheza na kupeperusha bendera ndogo za kitaifa wakifuatilia miziki ya bendi.

"Ni kijana mwenzetu! Najua atatuletea fursa zaidi," alisema dansa Juma Dominic huku yeye na kundi lake wakijiandaa,.

Idara ya taifa ya Polisi ilikuwa imeandika kwenye Twitter kwamba uwanja huo ulikuwa umejaa saa 11 alfajiri na kuwataka raia kukaa nyumbani, lakini umati wa watu uliendelea kujaribu kuingia kwa nguvu. Huduma ya Ambulance ya St John ilisema imewapeleka watu kadhaa waliojeruhiwa hospitali.