Waziri wa uchukuzi nchini Kenya aomba radhi baada ya umeme kukatika katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta

Ndege za Kenya Airways kwenye uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta

Waziri wa uchukuzi wa Kenya Jumamosi aliomba radhi baada ya umeme kukatika katika maeneo mengi Ijumaa usiku na kuwafanya abiria katika uwanja mkuu wa ndege jijini Nairobi kusumbuliwa na giza.

Umeme ulikatika Ijumaa katika maeneo mengi ya nchi saa tatu na dakika 45, kampuni ya kusambaza umeme ya KPLC ilisema katika taarifa, hitilafu hiyo ilisababishwa na tatizo la mfumo.

Kanda ya video kwenye mtandao wa kituo cha utangazaji cha NTV iliwaonyesha wasafiri wakiwa wamesongamana karibu na mlango mkuu kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta huku kukiwa na giza, na wengine wakitumia taa za simu zao za mkononi kuangaza njia yao.

Mamlaka ya viwanja vya ndege ya Kenya(KAA) ilisema kuwa moja ya jenereta zake za dharura, ambayo inasambaza umeme katika mlango huo mkuu, haikufanya kazi baada ya umeme kukatika.

Jenereta zinazosambaza umeme kwenye mnara wa kuongoza safari za ndege na kwenye uwanja wa ndege zilifanya kazi muda wote, alisema waziri wa uchukuzi Kipchumba Murkomen katika mkutano na waandishi wa habari, akiongeza kuwa hakuna abiria au ndege zilizokuwa hatarini kutokana na hitilafu hiyo.

“Nataka niwaombe radhi wasafiri wote na watumiaji wa viwanja vya ndege ambao waliathiriwa kwa njia moja au nyingine na kutakika kwa umeme,”Murkomen alisema.