Watu wawili wameuawa katika maandamano ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Msumbiji, ambapo polisi waliwafyatulia risasi waandamanaji katika miji kadhaa, shirika lisilo la kiserikali limesema Ijumaa.
Chama kikuu cha upinzani kiliitisha maandamano baada ya matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 11 kutangazwa na maafisa wa uchaguzi jana Alhamisi, yakionyesha chama tawala cha FRELIMO kilishinda katika mitaa 64 kati ya 65.
Maandamano yalifanyika katika mji mkuu Maputo na miji ya kaskazini ya Nacala na Nampula, huku polisi wakiwafyatulia risasi waandamanaji katika mitaa mingine kadhaa, kulingana na kituo cha kuhamasisha uadilifu wa umma (CIP).
Shirika hilo lisilo la kiserikali limesema pia mtu mmoja alipigwa na kuuawa na kifaa butu huko Nacala, na kuongeza kuwa watu wawili akiwemo mtoto wa miaka 10 walipigwa risasi na kujeruhiwa katika maandamano katika mji huo.