Hichem Abu Chkiouat, waziri wa usafari wa anga katika utawala unaongoza mashariki mwa Libya, ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu kwamba uamuzi wa kuwafukuza waandishi wa habari kuondoka mjini humo hauhusiani na maandamano ya Jumatatu.
Amesema “Ni katika hali ya kujaribu kuweka mazingira bora kwa timu za uokoaji kufanya kazi yao kwa urahisi na kwa ufanisi.”
Ameongeza kuwa “idadi kubwa ya waandishi wa habari imekuwa kikwazo kwa kazi ya timu za uokoaji.”
Maandamano ya Jumatatu yalikuwa ya kwanza kuripotiwa katika mji wa Derna tangu ulipokumbwa na janga baya sana kuwahi kutokea katika historia ya Libya wiki moja kabla.
Mitambo ya mawasiliano katika mji huo, ambayo iliendelea kufanya kazi licha ya mafuriko, ilifungwa Jumanne asubuhi.
Maelfu ya watu wamethibitishwa walifariki na maelfu ya wengine haijulikani walipo kutokana na mafuriko ya Septemba 10, wakati mabwawa yalipopasuka mjini humo kutokana na kimbunga, na kusababisha dimbwi la maji ambayo yaliusomba mji huo.