UM wasema hali ya Sudan inahatarisha mamilioni ya watu

Umoja wa Mataifa na mashirika ya kimataifa yanaonya maisha ya mamilioni ya watu wa Sudan yamo hatarini huku ulimwengu ukifumbia macho mahitaji makubwa ya kibinadamu yanayoikabili nchi hiyo yenye vita.

Sudan imevumilia mwaka wa vita, ambao mashirika ya kibinadamu yanakubali kuwa ni moja ya majanga mabaya zaidi duniani yanayosababishwa na mwanadamu.

Shirika la Afya la dunia (WHO) linasema vita hivyo vimesababisha maafa makubwa kwa binadamu na vifo vya zaidi ya 15,000 vimeandikishwa huku watu 33,000 wakijeruhiwa.

Idadi ya wathirika walioripotiwa inaweza kuwa ya chini, msemaji wa WHO Christian Lindmeier, aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva, Ijumaa.

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, watu 20,000, nusu yao wakiwa watoto, wanalazimika kukimbia makazi yao nchini Sudan kila siku.