Ukraine kupewa F-16 kupambana vilivyo na Russia

Ndege ya kivita ya F-16 ikipokea mafuta kutoka angani. Ndege hiyo ina uwezo wa kudondosha mabomu kwa uhakika mkubwa palipo na adui.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema kwamba rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, amemhakikishia vya kutosha kwamba jeshi la Ukraine halitatumia ndege za kivita aina ya F-16 kuingia katika mipaka ya Russia.

Biden amewaambia waandishi wa habari mjini Hiroshima, Japan, kwamba ndege hizo za kivita F-16, zitatumika katika sehemu za Ukraine, kulipo na wanajeshi wa Russia.

Amesema kwamba huenda ndege hizo zisitumike katika mashambulizi ya jeshi la Ukraine katika wiki zijazo, lakini wanajeshi hao watazihitaji kujilinda dhidi ya wanajeshi wa Russia katika sehemu ambazo hawawezi kufika.

Viongozi wa nchi 7 zenye uchumi mkubwa, katika mkutano wao leo Jumapili, wamesema kwamba wataendelea kutoa misaada kwa Ukraine.

Biden ametangaza msaada wa kijeshi wa kiasi cha dola milioni 375 kwa ajili ya Ukraine, pamoja na magari ya kivita, wakati wa kufunga mkutano huo.