Ukraine inasema imetungua ndege 16 zisizo na rubani za Russia

Watu wakitizama ndege zisizo na rubani za Russia mjini kati Kyiv, Ukraine, Juni 15, 2023.

Ukraine ilizitungua ndege 16 zisizo na rubani za Russia kati ya 30 usiku wa kuamkia leo katika mkoa wa Cherkasy, jeshi lake la anga limesema Jumapili.

“Nyakati za usiku, adui alishambulia sana mkoa wetu wa Cherkasy kwa kutumia ndege zisizo na rubani, kwa bahati mbaya miundombinu ya viwanda katika mji wa Uman ilipigwa,” Gavana wa Cherkasy Ihor Taburets alisema kwenye mtandao wa Telegram.

Katika mkoa wa Zaporizhzhia nchini Ukraine, mtu mmoja aliuawa na mwingine kujeruhiwa katika shambulio la kombora la Russia.

Wizara ya ulinzi ya Uingereza ilisema katika taarifa yake ya kijasusi ya kila siku kwamba “nyaraka zilizovuja za wizara ya fedha ya Russia” zinadai kuwa Russia imejiandaa kuongeza matumizi yake ya ulinzi.

Bajeti ya wizara ya ulinzi ya mwaka 2024 iliyopendekezwa ni kiasi cha dola bilioni 110, ikiwa ni ongezeko la asilimia 68 ikilinganishwa na mwaka 2023, kulingana na nyaraka hizo.