Wahamiaji wahamishiwa sehemu nyingine mjini Paris

Mhamiaji akisindikizwa na polisi kutoka kwenye shule ya sekondari ya Jean-Jaures mjini Paris.

Polisi wa Ufaransa wametumia gesi ya kutoa machozi kwa waandamanaji pale maafisa walipokuwa wakiwahamisha wahamiaji kutoka shule moja mjini Paris humo ambapo wamekuwa wakipatiwa hifadhi.

Takriban wahamiaji 150 walikuwa wamechukua hifadhi kwenye shule ya Jean Jaures ilioko kaskazini mashariki mwa Paris wakati ikiwa haitumiki kutokana na ukarabati uliokuwa ukiendelea.

Polisi hivi leo waliwalazimisha kuondoka kwenye jengo hilo. Waliokuwa ndani walifunga milango wakati waandamanaji wakijaribu kuzuia kuingia ndani kutoka nje.

Mkuu wa polisi mjini Paris Michel Cadot amelidhibitishia shirika la habari la AP kuwa maafisa walitumia gesi hiyo kutawanya waandamanaji. Ameongeza kusema kuwa wahamiaji hao wamehamishiwa kwenye sehemu walizotengewa huku wakishauriwa kuomba hifadhi. Wakati huo huo, huenda mataifa ya ulaya yakatozwa faini iwapo yatakataa kupokea wahamiaji waliofurika barani humo wakitafuta hifadhi.