Chama tawala cha Georgia Dream, kilishinda kwa asilimia 54 ya kura zilizopigwa kulingana na tume ya uchaguzi, idadi ambao inakipatia wingi kwenye bunge. Upinzani umedai kuwa uchaguzi huo uliibwa, wakati mataifa ya Magharibi pamoja na waangalizi wa kimataifa wakieleza wasi wasi wao, wakidai kulikuwa na unyanyasaji wa wapiga kura, kununuliwa kwa kura, upigaji kura mara mbili pamoja na ghasia kwenye baadhi ya maeneo.
Upinzani mapema wiki hii uliandamana kwenye barabara za mji wa Tbilisi, wakati ukifanya mkutano wa kukemea matokeo hayo ambayo yametoa muhula mwingine kwa chama tawala. Waendesha mashitaka wamemuita Rais Salome Zourabichvili, ambaye anahusishwa na upinzani unaoungwa mkono na Magharibi kutoa ushahidi wake, lakini amehoji ni kwa nini anahitajika kutoa ushahidi wa wizi wa kura. “Siyo jukumu la Rais la kutoa ushahidi kuhusu wizi wa kura ,”aliambia wanahabari Jumatano.