Rais Kikwete ahahirisha mkutano wake na wazee wa jiji

Mgomo wa madaktari nchini Tanzania usio na kikomo umesababisha Rais Kikwete kuahirisha mkutano wake na wazee wa jiji

Mgomo wa madaktari unaoendelea katika hospitali za umma nchini Tanzania umesababisha Rais Kikwete kuahirisha mkutano wake na wazee wa jiji

Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Ijumaa aliahirisha mkutano wake na wazee wa mkoa wa Dar-es-salaam uliopangwa kufanyika Jumamosi ili kutoa nafasi zaidi ya kuweza kushughulikia kwa kina mgomo wa madaktari unaoendelea. Taarifa zaidi zinasema kuwa bwana Kikwete sasa atakutana na wazee hao siku ya Jumatatu jioni.

Huduma katika hospitali za umma jijini Dar es Salaam na baadhi ya mikoa nchini Tanzania bado zimezorota kufuatia madaktari kutangaza mgomo usiokuwa na kikomo ambao athari zake zimeanza kujionyesha moja kwa moja. Madaktari wanadai serikali iwapatie nyongeza ya mishahara na mazingira bora ya kufanyia kazi. Pia wanadai maafisa wa vyeo vya juu katika wizara ya afya na ustawi wa jamii Dr. Haji Mponda na naibu wake Dr.Lucy Nkya, waondolewe katika nyadhifa hizo kwa madai kuwa ndio chanzo cha matatizo.

Wakati huo huo imeelezwa kuwa mahakama kuu kitengo cha idara ya kazi imetoa uamuzi wa kusitishwa mara moja mgomo huo wa madaktari ulioitishwa nchi nzima tangu jumatano ya machi 7, mwaka huu.