Serikali-Kenya kuwadhibiti wanaotaka kuvuruga uchaguzi

Kenyatta and Raila

Serikali ya Kenya imesema kuwa itachukua hatua kali dhidi ya wale wote wanaotoa vitisho kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka wakati wakiendelea na maandalizi ya marejeo ya uchaguzi.

Vyanzo vya habari vimeeleza kuwa maafisa wa usalama wakutosha tayari wamejipanga katika maeneo mbalimbali ili kukabiliana na vitisho hivyo na serikali imesema itahakikisha usalama wa raia wake.

Kauli hiyo imetolewa na Rais Uhuru Kenyatta Ijumaa wakati Kenya ikiwa katika matayarisho ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Octoba 26.

Pia ametoa wito kwa wapiga kura kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo la uchaguzi

"Tunapojiandaa kwa uchaguzi wa urais tareje 26 Oktoba, ni muhimu kudumisha amani, sawa na tulivyofanya (Agosti) na awamu nyingine," amesema.

"Kupiga kura kuwachagua viongozi tunaowataka ni haki ambayo ilipiganiwa na mababu zetu, na lazima tuilinde."

"Sheria itatumika kwa njia sawa bila kujali hadhi yako katika jamii au siasa, hakuna atakayesazwa. Kwa wale wanaofana wakati wa vurugu, siku zenu zinafikia ukingoni, sheria itachukua mkondo wake na mtaadhibiwa ipasavyo."

Kiongozi huyo aliyasema hayo wakati wa kuadhimisha Siku ya Mashujaa ambayo hufanyika kila tarehe 20 Oktoba kuwakumbuka mashujaa waliopigania uhuru pamoja na Wakenya wengine waliotoa mchango wao wa kipekee kwa taifa hilo.

Kiongozi wa Muungano wa upinzani Nasa Raila Odinga amejitoa kutoka katika kinyang’anyiro cha marejeo ya uchaguzi huo na kusisitiza kuwa hakutambuwi uchaguzi huo.