Marekani yapinga Kagame kuwania awamu ya tatu

Rais wa Rwanda Paul Kagame

Marekani Jumamosi imelaumu uamuzi wa Rais Paul Kagame wa Rwanda kuwania awamu ya tatu ya urais mwaka 2017.

Katika taarifa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, John Kirby, alisema Marekani imesikitishwa na uamuzi huo, akisema Kagame "amepuuzia fursa ya kihistoria kuimarisha taasisi za kidemokrais ambazo wananchi wa Rwanda wamezifanyia kazi kwa bidii katika miaka 20 iliyopita."

Kagame alitangaza uamuzi wake katika hotuba ya televisheni Ijumaa, akisema, "Kutokana na umuhimu na uzito mliotumia kutafakari swala hili, sina la kufanya bali kukubali." Kagame, hata hivyo, aliongeza kuwa hadhani kuwa nia ya nchi hiyo ni kuwa na "rais wa maisha" na kusema asingependa kitu kama hicho.

Mwezi uliopita, wananchi wa Rwanda walipiga kura ya maoni kubadili katiba kumruhusu Kagame ambaye tayari ameongoza kwa awamu mbili agombee tena.

Jumatatu, Kagame alishukuru taifa kwa kupiga kura ya kubadili kiwango cha awamu za urais katika katiba, lakini wakati huo hakutoa fununu yoyote kwamba anapanga kugombania tena urais.