Rais wa Peru aondolewa madarakani kupitia kura ya bunge

Rais mpya wa Peru Dina Boluarte aliyekuwa makamu wa rais na kuchua nafasi ya rais Pedro Castillo aliyeondolewa madarakani na bunge. Dec. 7, 2022.

Bunge la Peru Jumatano limemuondoa madarakani rais Pedro Castillo, huku likipiga kura ya kumuweka makamu wa rais kwenye nafasi yake, muda mfupi baada ya kiongozi huyo kuidhinisha kuvunjwa kwa bunge muda mfupi kabla ya kuchukuliwa hatua ya kumuondoa madarakani.

Ofisi ya mpatanishi mkuu wa kitaifa imelitaja jaribio la Castillo la kuvunja bunge kama mapinduzi, ingawa mtaalam mmoja wa kisiasa ametofautiana na wazo hilo.

Eduardo Gamarra ambaye ni mtaalam wa sayansi ya siasa na pia mhadhiri kwenye chuo kikuu cha kimataifa cha Florida amesema kwamba bunge la Peru lina uwezo wa kumuondoa rais madarakani, wakati pia rais akiwa na uwezo wa kulivunja bunge, kwa hivyo hatua ya Castillo haikuwa mapinduzi.

Wabunge 101 dhidi ya 6 walipiga kura ya kuondolewa kwa Castillo kutoka ofisini kwa madai ya utovu wa maadili,wakati 10 hawakushiriki kupiga kura.