Rais Sirleaf awafuta kazi baadhi ya maafisa wake

Wahudumu wa afya wabeba maiti ya mwanamke aliyekufa kutokana na Ebola mjini Monrovia, Liberia

Liberia imeathiriwa sana na mlipuko wa Ebola ambao umesababisha vifo vya watu 2,400 katika Afrika Magharibi.

Rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf, amewafuta kazi maafisa 10 wakuu waliokiuka amri ya kurejea nyumbani kusaidia kupambana na ugonjwa wa Ebola. Maafisa hao wakiwemo manaibu wa mawaziri na makamishina waliagizwa tangu mwezi Agosti kurejea nyumbani lakini wakakaidi.

Liberia imeathiriwa sana na mlipuko wa Ebola ambao umesababisha vifo vya watu 2,400 katika Afrika Magharibi.

Kundi la kutoa misaada la madaktari wasio na mipaka limeeleza hali katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea kuwa tete kwa sababu nchi hizo hazina mifumo imara ya kutoa huduma za afya na hivyo hazina uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya wagonjwa wa Ebola.

Kirusi cha Ebola katika nchi hizo kimeuwa wafanyakazi wengi wa kutoa huduma za afya. Na huko Sierra Leone maafisa wamethibitisha kuwa daktari wa nne amefariki kutokana na Ebola.