NASA yaahirisha kuapishwa kwa Raila Odinga

Kiongozi wa upinzani Kenya Raila Odinga

Muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, umetangaza Jumapili kuwa unaahirisha mpango wa kumwapisha kiongozi wa upinzani Raila Odinga kama rais wa Kenya wiki hii.

Sherehe hizo zilizopangwa kufanyika mjini Mombasa Jumanne, ambayo ni siku ya Jamhuri nchini Kenya.

Taarifa ya kuahirishwa kwa sherehe hizo ilisomwa na Musalia Mudavadi mmoja wa viongozi wa juu wa muungano wa NASA. Mudavadi alifuatana na kiongozi mwingine pamoja na Gavana wa Makueni Kivutha Kibwana.

Sauti ya Amerika-VOA ilifanya mazungumzo na Ruth Wanjiku Njuguna juu ya tukio hili.

Your browser doesn’t support HTML5

Mahojiano ya VOA na Ruth Wanjiku Njuguna wa Radio Citizen, Kenya

NASA imesema imefanya uamuzi huo baada ya kujadiliana na pande mbali mbali nchini Kenya, na kusema kuwa sherehe ya kumwapisha Raila Odinga kama rais na Kalonzo Musyoka kama makamu wake itafanyika katika tarehe itakayotangazwa baadaye.

Kwa siku kadhaa zilizopita kumekuwa na shinikizo kubwa kwa NASA kufuta au kuahirisha sherehe hizo kwa hofu kuwa ingesababisha ghasia na machafuko nchini Kenya.

Marekani ilituma waziri wake mdogo anayeshughulikia maswala ya Afrika Nairobi wiki iliyopita Balozi Yamamoto ambaye alikutana na Raila Odinga na viongozi wengine wa Kenya katika juhudi za kufanya sherehe hizo zisimamishwe na upinzani ufanye mazungumzo na serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.