Maafisa wa Israel wanahoji baadhi ya maelezo, wakati Marekani ikitafuta uungaji mkono wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, katika kukubalika na kutekelezwa kwa makubaliano hayo. Pendekezo la Marekani ambalo VOA imeliona linaitaka Hamas kukubali na kutekeleza sitisho la mapigano bila kuchelewa na bila ya masharti.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Mathew Miller Jumatatu aliwaambia wanahabari kwamba Hamas ambayo ilipokea pendekezo la kusitisha mapigano Alhamisi wiki iliyopita, bado haijatoa majibu yake. Alisema kuwa sehemu kubwa ya mapendekezo hayo inaendana na pendekezo la Hamas lililotolewa wiki kadhaa zilizopita.
Baadhi ya mapendekezo kwenye mkataba wa sasa ni pamoja na wiki 6 za siltisho la mapigano, kuachiliwa kwa baadhi ya mateka waliopo Gaza, upelekaji wa malori 600 ya misaada kila siku kwa wapalestina, pamoja na kuendelea kwa mashauriano yanayolenga sitisho la kudumu kumaliza mzozo.