Myanmar kuachilia huru baadhi ya wafungwa wa kisiasa

Mya Aye (katikati) kiongozi maarufu wa wanafunzi nchini Myanmar akipokelewa na wenzake baada ya kuachuliwa huru NOV 17,2022

Serikali ya kijeshi ya Myanmar imesema kwamba itamuachilia huru mchumi, raia wa Australia Sean Turnell kutoka gerezani, miezi 21 baada ya kukamatwa kwake wakati jeshi lilipotekeleza mapinduzi na kuiondoa serikali iliyochaguliwa na raia mwaka uliopita.

Sean, na raia wengine watatu wa kigeni wameachiliwa kufuatia kile kimetajwa kama hatua ya nia njema kati ya Myanmar na Australia na ni sehemu ya mpango mpana wa kutoa msamaha kwa wafungwa.

Aliyekuwa balozi wa Uingereza Vicky Bowman na mumewe Ko Htein Lin, pamoja na mtengenezaji wa filamu wa Japan Toru Kubota, wanatarajiwa pia kuachiliwa huru.

Vyombo vya habari vya Myanmar vinaripoti kwamb msamaha huo ulitolewa katika maadhimisho ya siku ya kitaifa nchini Myanmar.

Turnell ambaye alikuwa mshauri wa uchumi wa rais wa Myanmar aliyeondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi Aung San Suu Kyi, alihukumiwa kifungo cha miaka 3 gerezani mnamo mwezi Septemba kwa kukiuka sheria ya siri za serikali. Amekanusha madai hayo.