Mwili wa mwanatelevisheni wa Uingereza aliyetoweka wapatikana Ugiriki

Mwanahabari na daktari wa Uingereza Michael Mosley aliyepatikana akiwa amekufa Jumapili Uingereza.

Mwili wa mtangazaji wa televisheni wa Uingereza, Michael Mosley umepatikana kwenye kisiwa cha Ugiriki Jumapili asubuhi, baada ya kutafutwa kwa siku kadhaa, familia yake imesema.

Msemaji wa polisi ambaye hakutaka kutajwa jina kutokana na uchunguzi unaoendelea, amesema kuwa mwili huo umepatikana kwenye ufukwe wenye mawe mengi, na kwamba unasubiri kutambuliwa.

Mke wake amesema katika taarifa kuwa Mosley alichukua njia tofauti wakati wa matembezi na kisha kuzirai kwenye eneo ambalo mwili wake usingepatikana kwa urahisi. Amekuwa akitafutwa tangu Jumatano kwenye kisiwa cha Symi.

Meya wa kisiwa hicho Lefteris Papakalodoukas, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba alikuwa kwenye boti akiwa na wanahabari pale walipoona mwili huo ukiwa mita 20 kutoka kwenye ufukwe wa Agia Marina.

Ameongeza kusema kuwa huenda Mosley alianguka kwenye bonde lenye mawe na kisha kukwama kwenye uzio. Ripoti zinasema kuwa wakati wa operesheni ya kuutoa mwili wake, afisa mmoja wa polisi pia alianguka na kuumia kiasi cha kupelekwa hospitali.