Malawi: Makamu rais akamatwa kwa tuhuma za rushwa

Makamu rais wa Malawi Saulos Chilima

Idara ya kupambana na rushwa nchini Malawi imemkamata makamu rais wa nchi hiyo Saulos Klaus Chilima kwa tuhuma za rushwa, idara hiyo imesema leo Ijumaa.

Chilima atafikishwa mahakamani ambapo anatarajiwa kushtakiwa. Anakabiliwa na makosa matatu ya vitendo vya ulaji rushwa, kati ya mashtaka mengine, taasisi hiyo ya kupambana na ufisadi imesema katika taarifa.

Mawakili wa Chilima hawakupatikana mara moja ili kutoa maelezo zaidi, Reuters imesema.

Taarifa hiyo inadai Chilima alizawadiwa kwa kuzisaidia kampuni za Xiavar Limited na Malachitte FZE, kampuni mbili zilizounganishwa na mfanyabiashara raia wa Uingereza Zuneth Sattar kupewa kandarasi na serikali ya Malawi.

Idara hiyo ya kupambana na ufisadi imekuwa ikimchunguza Sattar na maafisa wengine wa umma nchini Malawi kwa tuhuma za uporaji wa rasilimali za serikali kwa kushawishi utoaji wa kandarasi kupitia mfumo wa zabuni ya umma nchini humo, idara hiyo imesema.